MAELEZO YA KITABU
Saida, mke wa Omari, yuko kitandani na mpenzi wake Abdallah, ambaye hataki
kumuacha hadi aahidi kwenda kwake siku moja. Wakati huohuo, Omari anarudi
kutoka kazini na Abdallah anajificha uvunguni. Baada ya Omari kuingia, Saida
anatafuta kisingizio cha kumtoa nje ili kumpa Abdallah upenyo wa kutoroka. Sio
tu kwamba anafanikiwa kufanya hivyo, pia anapata kibali cha kutekeleza ombi
lake la kwenda kumtembelea mama yake anayedai kuwa ni mgonjwa kijijini. Hata
hivyo, dakika chache baada ya Saida kuondoka, Abudu analeta taarifa ya kifo cha
mama Saida. Anamjulisha Omari na hatimaye, wote wawili wanaondoka kwenda
kwenye mazishi. Huko mazishini, Saida aliyeaga kwenda kumwona mama yake
hayupo na hafiki hadi shughuli ya mazishi inakamilika. Baada ya Omari kurudi
nyumbani, Saida anarudi akiwa na furaha, akimletea Omari matunda na salamu
kutoka kwa mama yake 'aliyepona'. Soga yake ya furaha inakutana na ukimya wa
kuogofya; mwishowe, Omari anamjulisha kwa ukali kifo na mazishi ya mama
yake siku kadhaa zilizopita.