Profesa Ebrahim Hussein ni mwanafikra wa Kiswahili, msomi, mshairi, mtunzi wa tamthiliya na mwandishi wa matukio ya kihistoria na kisiasa wakati wa ukoloni Afrika na baada ya uhuru. Mchango wake katika fasihi ya Kiswahili, hasa katika tamthiliya na sanaa za maonesho unamfanya kuwa miongoni mwa vinara wa fasihi ya Kiswahili Afrika Mashariki.
Ebrahimu Hussein, Profesa Penina Muhando na Profesa Amandina Lihamba, wanatambulika kama waanzilishi wa tamthiliya ya majaribio ya Kiafrika, ambayo sasa ni utanzu kamili na uga thabiti. Ebrahim Hussein alizaliwa tarehe 5/6/1943 huko Kilwa mkoani Lindi, nchini Tanzania wakati wa ukoloni wa Waingereza. Alisoma shule ya msingi mkoani Lindi na
baadaye kuhamia shule ya Aga Khan jijini Dar es Salaam ambako alisoma hadi Kidato cha Sita. Mnamo mwaka 1966, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma Fasihi ya Kiswahili, Kifaransa, Sosholojia na Tamthiliya. Alihitimu mwaka 1969 na kupata shahada ya kwanza katika
sanaa (BA). Ebrahim Hussein ni miongoni mwa wanafunzi
wa kwanza kusoma Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ambao baadaye walitwikwa jukumu la kuwa walimu
na wanazuoni wa kwanza wa kufundisha na kuendeleza lugha
na somo hilo. Mwaka 1970 Hussein alijiunga na masomo
ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Humboldt
nchini Ujerumani akibobea katika Tamthiliya na Sanaa za
Maonesho. Mwaka 1975 alihitimu na kupata shahada ya
uzamivu. Mwaka huohuo alirejea Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kuwa mhadhiri. Baadaye alipandishwa cheo na
kuwa Profesa. Mwaka 1985 aliacha kazi Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam.
Hussein aliibuka kuwa mtunzi wa tamthiliya mwaka 1967,
alipoandika na kuigiza Wakati Ukuta, takribani miaka 10
baada ya Graham Hyslop kuchapisha tamthiliya ya kwanza
ya Kiswahili, Afadhali Mchawi na Mgeni Karibu na Henry Kuria
kuchapisha Nakupenda Lakini... (Hyslop alikuwa Mwingereza
aliyekuwa akifanya kazi katika serikali ya kikoloni nchini
Kenya na H. Kuria alikuwa mwanafunzi wake). Tamthiliya ya
Wakati Ukuta inaonesha, mambo mbalimbali lakini wazo kuu
ni mgogoro kati ya kizazi cha kisasa na kizazi kilicho shikilia
jadi. Kazi hii ilimfanya Ebrahim Hussein kujitambulisha
kama mtunzi mahiri wa tamthiliya ya Kiswahili. Mwaka
huohuo Hussein aliandika Alikiona, ambayo inaangazia suala
la ukosefu wa uaminifu katika ndoa. Kinjeketile ilifuata mwaka 1969, tamthiliya inayohusu mapambano ya wenyeji wa Kusini
mwa Tanganyika dhidi ya utawala wa Wajerumani wakati wa
ukoloni (Vita vya Majimaji 1905-1907). Kazi hii ilitafsiriwa
kwa Kiingereza mnamo mwaka 1977 na kuigizwa katika
tamasha la FESTAC huko Lagos. Mashetani ilifuata mwaka
wa 1971. Kinjeketile na Mashetani ni mafumbo ya kisiasa
yanayoangazia hali na migogoro ya kijamii na kiuchumi
wakati na baada ya ukoloni barani Afrika. Jogoo Kijijini na Ngao
ya Jadi (1976) – zilichezwa jukwaani na mwigizaji mmoja (E.
Hussein) na zilitokana na ngano za jadi za Kiafrika; miaka
minne baadaye alichapisha Arusi – tamthiliya ya kisiasa
iliyoangazia muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Kwenye Ukingo wa Thim ilifuata mwaka 1988. Tamthiliya hii
inasawiri, mbali ya mambo mengine, changamoto za kujenga
na kuendeleza ‘utaifa’ linalojumuisha watu wa makabila
mbalimbali ambao hawakuwa wanaaminiana.
Kazi za Ebrahim Hussein zinasifika kwa matumizi ya lugha
ya kificho na mafumbo yanayododosa hali ya kijamii na
kisiasa barani Afrika, mara nyingi zikiangazia hali katika
jamii ya Kitanzania baada ya ukoloni. Pia zinatambulika kwa
utajiri wa lugha na matumizi ya ushairi wa kisasa kuwasilisha
mawazo na hisia changamano. Kazi za Hussein zinadhihirisha
mtazamo wake mpana na msimamo thabiti katika kutetea
utamaduni, historia na utambulisho wa Mwafrika. Kwa
muda mrefu kazi za Hussein zimesomwa katika shule na
vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika.
Ubunifu wa Hussein katika matumizi ya lugha na katika umbo vimechangia kwa sehemu kubwa fasihi ya Kiswahili
na tathmini ya kijamii ya hali ya kisasa barani Afrika.
Kwa miongo kadhaa, kazi na mafundisho ya Hussein
vimehamasisha waandishi wa tamthiliya, washairi na wasomi
kutambua nafasi ya Kiswahili katika kukuza utambulisho wa
Mwafrika na kueneza utamaduni wake. Tasnifu yake kuhusu
Tamthiliya ya Tanzania imesalia kuwa maandishi ya msingi ya
kuelewa mabadiliko ya tamthiliya ya Kiswahili.
Ebrahim Hussein ni mbuji katika fasihi ya Kiswahili na
Kiafrika ukanda wa Afrika Mashariki na ni miongoni mwa
wanaharakati mashuhuri wa Kiswahili duniani. Ingawa
uamuzi wake wa kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha
yake kuu ya kuandikia kazi za fasihi huenda ulimnyima
fursa ya kutambulika katika jukwaa la kimataifa kwa muda
mrefu. Ni dhahiri kuwa, mchango wake adhimu umekiweka
Kiswahili katika ramani ya dunia na kukipa thamani kubwa
ulimwenguni kiasi ambacho, kazi zake zitaendelea kung’ara
na kutambulika kama nguzo imara zilizojenga lugha hii
adhimu barani Afrika.