BOOK OVERVIEW
Diwani ya Mkanyaji ni kazi maridhawa ya ushairi wa Kiswahili. Kama inavyofahamika pasi shaka kwamba, ushairi ndio utanzu wa awali miongoni mwa nyinginezo katika fasihi ya Kiswahili kuibushwa na binadamu katika harakati za kupambana na mazingira yake ya wakati huo. Katika diwani hii, mtunzi anazitumia mbinu anuai za kifani katika kuyaeleza makusudi yake. Ingawa Mkanyaji si mzee lakini amejikusuru sana kutumia lugha pevu aliyoibebesha maudhui komavu kwa mnasaba wa jamii hasa jamii ya Waswahili. Kazi hii ingawa ilifanya subira ya muda mrefu hadi kutoka sasa lakini kwa hakika ina ukale mwingi hasa kwa kutilia maanani lugha yake ambayo imeyafumbata maudhui mengi ya kiimani, falsafa, kijamii na kijamaa. Ukale uliojumuishwa kwenye diwani hii, imeifanya kazi hii kutokumchosha msomaji mpenda mashairi ganda na kiini chake. Kwa hiyo, kwa kadri atakavyoendelea kusoma shairi moja baada ya jingine, ndivyo itakavyomwongezea hamu na ghamu ya kuendelea kuchota maarifa yaliyomo humu.