BOOK OVERVIEW
Mukwava wa uhehe ni Tamthiliya ya kihistoria inayoangazia matukio muhimu ndani ya himaya ya Mukwavinyika wa Uhehe katika kipindi cha uvamizi wa Wajerumani, katika ardhi ya Tanganyika kati ya mwaka 1891 – 1898.
Ingawa vitabu vingi vinamtambua kiongozi huyu wa Uhehe kama mkwavi au Mkwavinyika jina hili linaandikwa hivyo kutokana na kuathiriwa na matamshi ya Wajerumani. Tamthiliya hii inasahihisha kosa hili la kikoloni kwa kutumia jina sahihi la mtawala huyu, Mutwa Mukwava.
Tamthiliya inaanza na ushindi wa jeshi la Mukwava dhidi ya wajerumanikatika bonde la Lugalo chini ya jemedari mwanamama Mutage Mwafyale. Kushinda kwa jeshi la Uhehe kunapelekea shangwe na vifijo katika Uhehe yote na mshtuk, hofu na fedheha katika kambi ya Wajerumani iliyoko pwani ya Dar es Salaam. Mbali na ushindi huu mkubwa, hapakosekani chokochoko kati ya washauri wa Mukwava kujaribu kufanya usaliti kwa kutoa taarifa za siri kwa Wajerumani. Mtu huyu anapoumbuliwa anahukumiwa adhabu ya mwisho ambayo ambayo Mukwava mwenyewe anaamua kuitekeleza. Hili nalo linaibua uhasama na hasira kati ya baadhi ya watendaji wa Mukwava. Hasira hii inazaa chuki na utengano ambao mwishoni unaleta ufa katika himaya ya Uhehe. Utawala wa Wajerumani unatumia ufa huu kujaribu kwa mara nyingine kuishambulia Uhehe ya Mukwava. Mashambulizi haya yanarindima na kukolea lakini hayabadilishi msimamo na uzalendo wa wapiganaji wa Uhehe. Wapiganaji wa Mutwa wanapigana kufa na kupona kulinda ardhi yao na kukataa katukatu kusaliti na kurudi nyuma.
Tamthiliya hii, mbali na kukufurahisha na kuhuzunisha, itakujulisha usiyoyajua juu ya mtawala huyu shujaa aliyeshangaza Ujerumani hadi kumfanya mtawala wa Ujerumani kutaka fuvu lake lisafirishwe Kwenda Ujerumani baada ya yeye kujiua.
|
|