BOOK OVERVIEW
Mwanzoni mwa miaka ya 1970 palitokea mgogoro wa ushairi nchini Tanzania na Kenya. Makundi mawili, yaliyoitwa “wanamapokeo” na “wanausasa”, yalibishana magazetini, vitabuni na kwenye makongamano kuhusu maana na maumbo ya ushairi. Miongoni mwa matokeo mazuri ya mgogoro huo ni kuandikwa na kuchapishwa kwa makala mengi na vitabu kadha vya nadharia na mikusanyo ya ushairi. Diwani hii ya Malenga wa Bara ni tunda mojawapo la mgogoro huo. Watunzi wa mashairi yaliyomo humu, K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi, walikuwa miongoni mwa waanzilishi na washiriki wakubwa wa mgogoro huo. Hivyo mashairi yao yenye maumbo na miundo mbalimbali ya “kimapokeo” na ya “kisasa”, ni kielezo cha vitendo cha nadharia yao ya ushairi. Aidha, mashairi haya yanaakisi vizuri vuguvugu na mikikimikiki ya kisanaa, kijamii na kiitikadi ya miaka hiyo ya 1970.